Saturday, December 24, 2016
KINGUNGE ASEMA BILA TUME HURU WAPINZANI WASAHAU KUINGIA IKULU
Do you like this story?
Mwanasiasa
mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amesema bila ya kuwa na tume huru ya
uchaguzi na Katiba Mpya, vyama vya upinzani visahau kushinda urais katika
Uchaguzi Mkuu ujao.
Kauli
ya Kingunge imekuja siku moja baada Rais John Magufuli kumteua Jaji
Themistocles Kaijage kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
baada ya Jaji Damian Lubuva kufikia muda wake wa kustaafu.
Kwa
muda mrefu, NEC imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kwa kutokuwa huru
kwa sababu ya uongozi wake wote huteuliwa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa
CCM, huku sheria zikikataza matokeo ya nafasi ya urais kupingwa mahakamani.
Mbali
na mwenyekiti kuteuliwa na Rais, wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ni
wakurugenzi wa wilaya ambao pia huteuliwa na Rais kwa kuwa NEC haina wafanyakazi
wake kote nchini.
Akizungumza
katika mkutano wa kuwafariji vijana waliokamatwa na Jeshi la Polisi na
kushtakiwa kwa makosa yaliyohusu Uchaguzi Mkuu uliopita, uliofanyika jijini Dar
es Salaam jana, Kingunge aliwatia moyo vijana hao, akisema hakuna ushindi
unaopatikana bila kupambana.
Kingunge,
aliyetumia muda mrefu kueleza historia ya maisha yake katika siasa na jinsi
alivyopambana katika harakati za kudai uhuru, alisema hali ya sasa ni mbaya
kuliko wakati wa wakoloni wa Kiingereza ambao walikujwa wakali, kwa sababu CCM
haifuati Katiba wala sheria.
“Yako
mambo ambayo itabidi tujitahidi yaamuliwe sasa kabla ya 2020. Mambo hayo
makubwa kwanza ni tume huru (ya uchaguzi). Suala hilo lazima lizungumzwe sasa,
hatuwezi kwenda 2020 na tume ya sasa na Katiba ya mwaka 1977. Tukienda hivyo
sahau habari ya upinzani kushinda uchaguzi,” alisema.
Kingunge
ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo ya waziri
anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na mkuu wa
mkoa alisema, “(Pia) Sheria inayohusu matokeo ya uchaguzi wa Rais kuhojiwa.
Hivi sasa sheria inasema matokeo ya uchaguzi wa Rais hayahojiwi mahakamani.
Lazima hilo suala lipate jibu sasa. Kwa hiyo Katiba na sheria iseme, matokeo ya
uchaguzi wa Rais yanaweza kuhojiwa mahakamani. Tusipokuwa na hilo, tutakuwa na
matatizo makubwa sana.”
Alisema
pamoja na kwamba Chadema inapendwa na wananchi wengi na Edward Lowasa
aliyegombea urais kwa tiketi chama hicho, anapendwa, bado ni vigumu kushinda
kwa sababu mfumo uliopo sasa.
“Tufanye
yoyote, lakini tuhakikishe, ama tunapata Katiba Mpya au vipengele hivi vya
sheria vinafanyiwa marekebisho. Kwa maoni yangu, kundi hili lililo madarakani
bila shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi, halitataka mabadiliko,” alisema.
Alisema
enzi zao walifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitolea kwa nguvu na wengine,
na yeye akiwamo, waliacha kazi za mishahara mikubwa na kujiunga na Tanu
kupigania uhuru.
“Tulifanikiwa
kupata uhuru kwa sababu walijitoa mhanga. Wengi tu waliacha kazi, mtu anamaliza
chuo kikuu anasema sitaki kazi anaingia Tanu kusaidia. Kwa hiyo tukawa na jeshi
kubwa la vijana waliohakikisha nchi inapata uhuru,” alisema.
“Ninyi
mnapambana katika mazingira magumu na wazee wenzenu walipambana katika
mazingira hayo. Haikuwa rahisi. Wapo wengi walitusaliti, wengine hawakufanya
lolote. Baba yangu tuligombana, nilipoacha kazi kwenda kuitumikia Tanu. Miezi
sita hatukuzungumza.”
Akizungumza
mkutano huo, Lowassa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwatia moyo
vijana walioshtakiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, akisema bado jeshi
kubwa la vijana linahitajika.
“Yaliyopita
si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo. Si haki kusema unakwenda mahali pengine,
mwenzako amepasafisha, safisha pa kwako. Nimefurahia moyo huo. Kama alivyosema
Ngombale, tunataka jeshi kubwa zaidi, watu wengi zaidi,” alisema Lowassa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “KINGUNGE ASEMA BILA TUME HURU WAPINZANI WASAHAU KUINGIA IKULU”
Post a Comment