Saturday, December 24, 2016
SERIKALI YAPIGA MARUFUKU SHULE BINAFSI KUCHUJA NA KUFUKUZA WANAFUNZI
Do you like this story?
Serikali imepiga marufuku utaratibu wa shule binafsi kuendesha
mitihani ya mchujo kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya kitaifa ili
shule zao ziweze kuongoza kwa kubaki ma wanafunzi wazuri(walio na uwezo mzuri
darasani)
Agizo hilo pia linapiga marufuku kuwafukuza shule wanafunzi
wanaoshindwa mitihani ya mchujo,kuwasajili kama private candidate wale
wanafunzi wanaofeli mitihani hiyo,kuwahamisha shule au kuwakaririsha madarasa.
Kibano kipya chaja kwa shule binafsi
Hiyo ni baada ya kutangaza kupiga marufuku utaratibu wa kuwachuja
wanafunzi wanaotakiwa kufanya mitihani ya taifa uliokuwa unaofanywa na baadhi
yao kwa lengo la kuonekana shule zao zinafaulisha vizuri.
Hivi karibuni, Nipashe iliripoti kuhusu hofu ya baadhi ya shule
hizo; za msingi na sekondari ziko hatarini kubadilishwa matumizi kutokana na
kukosa wanafunzi wa kutosha baada ya Serikali kuboresha shule zake na kutoa
elimu bure, huku hali ya kiuchumi ikiwaumiza wananchi.
Huku udahili kwenye shule za serikali ukiongezeka na kuonekana
kuwa tishio kwa ustawi wa shule za watu na taasisi binafsi, imewabana tena
wamiliki wa shule binafsi kwa kuwazuia kufanya mchujo wa wanafunzi wanaoingia
kwenye madarasa au vidato vyenye mitihani ya taifa.
Mmoja wa wazazi aliliambia Nipashe kuwa mwanawe anayesoma kidato
cha tatu katika shule moja ya binafsi jijini Dar es Salaam, amepangiwa
kuhamishiwa shule nyingine ya mmiliki huyo huyo kutokana na kufaulu kwa daraja
la tatu.
Kwa mujibu wa mzazi huyo, kuna wanafunzi takribani 70 wa kidato
cha tatu, wanatarajiwa kuhamishwa katika shule hiyo waliyosajiliwa tangu kidato
cha kwanza, watahamishwa shule hiyo na kubaki wale waliofaulu kwa viwango vya
madaraja ya kwanza na pili tu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk.
Leonard Akwilapo, akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam juzi, alisema ni
marufuku shule kumkaririsha darasa, kumfukuza, kumhamishia shule nyingine au
kumsajili kama mtahiniwa binafsi (PC) mwanafunzi kwa kigezo cha kutofanya
vizuri katika mitihani ya shule husika.
“Ni marufuku kabisa kufanya hivyo. Mitihani tulionayo sisi (Wizara
ya Elimu) ndiyo mchujo sahihi. Na mtihani ambao unamkaririsha mwanafunzi ni
mtihani wa taifa wa kidato cha pili na mtihani wa darasa la nne tu,” alisema.
“Wala siyo mtihani wa shule na madarasa mengine hayana mtihani wa
kumkaririsha mtoto au kumfanya aondolewe shuleni au ahamishiwe shule nyingine,
hatuna utaratibu huo na serikali haiwezi kukubaliana nao,” aliongeza Dk.
Akwilapo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi
(Tamongosco), Benjamin Nkonye, aliiambia Nipashe jana kuwa utaratibu
wanaoutumia ni kushauriana na wazazi wa wanafunzi wanaoshindwa kufanya vizuri
shuleni ikiwamo kuwapeleka katika vyuo vya ufundi (Veta).
Alisema shule binafsi zinapaswa kupongezwa kwa kudahili hata
wanafunzi hasa wa sekondari ambao shule za serikali huwa haziwachukui kutokana
na kushindwa kufanya vizuri katika mitihani ya shule za msingi.
“Hakuna shule ambazo zinapaswa kupongezwa kama za binafsi,
serikali yenyewe imekuwa ikichagua wanafunzi wote. Inatuachia ‘vilaza’, lakini
sisi kwa kujitoa kuwasaidia watoto wa Kitanzania, tunakubali kuwachukua hao hao
wanaoonekana wabaya, tunawafundisha na mwisho wa siku wanakuwa wazuri kuliko
hata hao wanaokuwa wamethaminiwa na serikali,” alisema Nkonya.
“Na sisi hatuchuji wala kumfukuza mwanafunzi, isipokuwa
kinachofanyika kwa kuwa tunapokea wakati mwingine wanafunzi ambao ni ‘vilaza’
kabisa, huwa tunawagawanya katika makundi kulingana na uelewa wao, wenye uelewa
wa kwanza, wa kati na wa mwisho. Na mwisho na tunawafundisha kulingana na
‘speed’ (kasi) ya uelewa wao na wanajikuta wanafanya vizuri.
“Lakini kwa sababu sisi tunakuwa na wanafunzi ambao ni wagumu
sana, inapoonekana wakatokea wachache hawawezi kabisa huwa tunashauriana na
wazazi wao, kuwapeleka Veta ili kule wanapokuwa wanaendelea kujifunza, wengine
wanafanya vizuri hadi wanafika vyuo vikuu, hatuwaachi kama ilivyo katika shule
za serikali na vyuo vya serikali, haya maneno mengine yanayozungumzwa ni ya kisiasa
tu.”
HALI ILIVYO
Uchunguzi wa Nipashe uliofanyika hivi karibuni katika baadhi ya
mikoa, ulibaini baadhi ya wamiliki wa shule binafsi wamekuwa na utaratibu wa
kuchuja wanafunzi kila mwaka kwa lengo la kupata wenye uwezo mkubwa darasani.
Ilibainika kuwa utaratibu huo umekuwa ukifanywa kwa nia ya kuwa na
wanafunzi wenye uwezo mkubwa ili shule hizo zifanye vizuri katika mitihani ya
taifa, hivyo kuvutia wazazi wengi zaidi kupeleka watoto wao.
Gazeti hili lilibaini kuwa, baadhi ya shule binafsi zimekuwa
zikiendesha utaratibu huo kipindi cha mitihani ya mwishoni mwa mwaka kwa
kuwafukuza, kuwakaririsha darasa au kuwahamishia shule nyingine wanafunzi
wanaoshindwa kufikia kiwango kinachowekwa na shule husika kwenye mitihani ya
kufunga mwaka.
Nipashe pia ilibaini baadhi ya shule hizo zimekuwa na utaratibu wa
kuwachuja kwa kuwasajili kama watahiniwa binafsi (Private Candidates) kwenye
mitihani ya taifa wanafunzi wake wanaoshindwa kiwango kilichowekwa wanapofanya
mitihani ya shule husika.
MTOTO WA PROFESA AKACHA KULA
Akizungumzia suala hilo katika mahojiano maalumu na gazeti hili
jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Masomo ya Shahada ya Kwanza Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Allen Mushi, alisema haungi mkono utaratibu wa
baadhi ya shule binafsi kuwafukuza wanafunzi wanaoshindwa kufikia kiwango cha
alama zilizojiwekea.
Alisema: “Ni makosa kumfukuza shule mwanafunzi aliyekuwa
amedahiliwa, anasoma halafu unamsitishia, unamwambia nenda katafute shule
nyingine.
“Na ni kweli wana tabia hiyo. “Nina kijana wangu yuko ‘Form One’
(Kidato cha Kwanza) anasoma shule … (anataja eneo ilipo shule hiyo), yaani
anasoma kupindukia. Nilikuwa na wasiwasi hata akija likizo hawezi kula vizuri,
anasoma tu.”
Alisema kuwa katika shule hiyo ya jijini Dar es Salaam anayosoma
mtoto wake, wameambiwa ni lazima awe na wastani wa kuanzia alama 50 katika
mitihani ya shule ili aruhusiwe kuingia kidato kinachofuata, vinginevyo
wakatafute shule nyingine.
“Katika utaratibu wa elimu, siyo sahihi kufanya hivyo, wewe kama
wanafunzi wameshindwa, wewe siyo ndiyo mwalimu, ndiyo kazi yako ya kufanya
wanafunzi waelewe,” alisema na kufafanua zaidi:
“Sasa ukiwa unafanya hivyo, mwisho wa siku utakuwa unafelisha
darasa zima na kujitamba kwamba unafaulisha kwa sababu umefukuza wengi na
kubaki na wazuri wachache. Sasa hiyo ni biashara, siyo elimu tena. Wewe kama ni
mwalimu, unatakiwa kufundisha wanafunzi wote.
“Kwa hiyo, wanasema shule za ‘private’ (binafsi) zinafaulisha
wanafunzi wote, kumbe wengine mliowachuja. Mimi binafsi sikubaliani na hali
hiyo kabisa.”
Alisema ni muhimu wizara yenye dhamana ya elimu nchini iweke
masharti kwamba ukishadahili wanafunzi, wasiondolewe shuleni kwa utaratibu wa
viwango vya ufaulu katika mitihani ya shule husika isipokuwa kwa sababu za
tabia mbaya na zisizofaa kwa mwanafunzi kwa mujibu wa sheria za nchi.
MAKUNDI YA UELEWA
Msomi huyo alisema wanafunzi wamegawanyika katika madaraja mawili
kiuelewa darasani, la kwanza likiwa la wenye uelewa wa haraka (fast learners)
na jingine likiwa la wenye uelewa hafifu (‘slow learners).
“Wote hao wanapaswa wazingatiwe katika elimu. Sasa hawa (shule
binafsi) wenyewe wanaangalia ‘fast learners’ tu. Ni vema wote wakachukuliwa
katika vigezo sawa, siyo unawachuja wengine halafu unasema unafaulisha wote,”
alisema Prof. Mushi.
BIASHARA
Aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mukoba,
akizungumza na Nipashe jana kuhusu changamoto hiyo, alisema si vyema kumfukuza,
kumkaririsha darasa au kumhamisha mwanafunzi aliyefanya vibaya katika mitihani
ya shule.
“Mtihani wa Kidato cha Pili ni mchujo sahihi tu. Shule binafsi
wanakosea. Ufundishaji wa kawaida huwezi kuwa na wanafunzi wanaopata daraja la
kwanza na la pili tu,” alisema.
“Hao shule binafsi kuna muda wanateleza kidogo, kwa sababu hakuna
mwanafunzi asiyefundishika labda kwa sababu wao wanataka suala la biashara. Ni
kuonea wanafunzi, bahati mbaya akishaanza shule ya ‘private’ (binafsi) kidato
cha kwanza, hawezi kurudi kwenye mfumo wa serikali, kwa hiyo wanafunzi
wanahangaika,” alisema zaidi Mukoba.
-Nipashe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SERIKALI YAPIGA MARUFUKU SHULE BINAFSI KUCHUJA NA KUFUKUZA WANAFUNZI”
Post a Comment