Friday, January 20, 2017
BILLIONI 2.4 KUBORESHA MRADI WA MAJI NJOMBE
Do you like this story?
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imetoa shilingi
bilioni 2.4 kwaajili ya kuboresha mradi wa maji katika mji wa Makambako mkoani
Njombe
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Januari 19, 2017) wakati
akizungumza na wananchi katika uwanja wa Polisi Makambako ulipofanyika mkutano
wa hadhara akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Njombe. Waziri Mkuu alisema
lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi za salama
katika umbali usiozidi mita 400 kama inavyosema sera ya maji.
Hata hivyo aliwataka wananchi kutofanya shughuli za kijamii katika
vyanzo vya maji ili kuvilinda. Alisema Serikali inatumia fedha nyingi kutafuta
maji kwa sababu vyanzo vingi zimekauka kutokana na shughuli za kibinadamu.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alizungumzia suala la madai ya
fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa kituo cha ukaguzi cha pamoja na soko la
kitamaifa katika eneo la Makambako aliahidi kuwa watalipwa.
“Fidia zenu mtalipwa hivi katibuni baada ya Serikali kupitia
Wizara ya Fedha na Mipango kukamilisha taratibu za ulipaji,” alisema. Wananchi
hao walilalamikia ucheleweshwaji wa malipo ya fidia hizo kupitia katika mabango
mbalimbali pamoja na mbunge wa Njombe, Mheshimiwa Deo Sanga.
Serikali imeanzisha eneo la Idofi lililoko Makambako kwa ajili ya
ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja wa magari ya mizigo ili kupunguza vikwazo
vya kibiashara barabarani kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kituo hicho kitakuwa na vituo vidogo vya Polisi, Uhamiaji, Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), Maliasili pamoja na vituo vya mizani.
Awali mbunge wa jimbo la Njombe Mheshimiwa Sanga alisema moja ya
changamoto inayowakabili wakazi wa mji wa Makambako ni ucheleweshwaji wa malipo
ya fidia kwa waliopisha ujenzi wa kituo hicho hali inayosababisha baadhi yao
kwenda kudai fidia hiyo kwake.
”Mheshimiwa Waziri Mkuu leo na sisi wananchi wa Makambako
tutapona. Baba Majaliwa hawa wananchi wanadai fidia yao kwa muda mrefu na
baadhi yao wamefikia hatua ya kuja kulala nje ya nyumba yangu wakigoma kuondoka
hadi niwape ufafanuzi wa malipo yao,” alisema.
Mbali na kuwasilisha changamoto hiyo mbunge huyo pia aliishukuru
Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada zake za kuboresha maendeleo ya wananchi
hususan wakazi wa jimbo la Njombe.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Njombe, Bw. Christopher Ole
Sendeka alisema Serikali imetenga sh. bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa daraja
la chuma lenye urefu wa mita 95 katika mto Ruhuhu.
Alisema mkataba wa ujenzi wa nguzo za daraja tayari umesainiwa
kati ya mkandarasi wa kampuni ya M/s Lukolo na Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS) kwa gharama ya sh bilioni 6.17 na muda wa utekelezaji ni miezi 24.
Akizungumzia mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi Bw. Ole Sendeka
alisema mkoa unaendelea na kampeni za upimaji, zilizowezesha watu kufahamu afya
zao na kuchukua tahadhari ya jinsi ya kujikinga na kuepuka maambukizi mapya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JANUARI 20, 2017.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BILLIONI 2.4 KUBORESHA MRADI WA MAJI NJOMBE”
Post a Comment