Thursday, January 19, 2017
MARUFUKU KULIMA, KUINGIZA MIFUGO NDANI YA VYANZO VYA MAJI-MAJALIWA.
Do you like this story?
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa
mikoa ya Singida, Mbeya, Iringa na Dodoma wawasimamie wananchi wao na
kuhakikisha hakuna shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya vyanzo vya
maji.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Januari 19, 2017)
alipozungumza na watumishi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Mtera alipotembelea
bwawa la Mtera akiwa njiani kwenda mkoani Njombe kwa ziara yake ya kikazi.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya Kaimu Meneja
wa Kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera, Mhandisi Edmund Seif kutaja baadhi ya
changamoto zinazokikabili kituo hicho kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa shughuli
za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu ameagiza vifanyike
kwa vikao vya ujirani mwema ili wananchi waelimishwe umuhimu wa kutunza vyanzo
vya maji na ni marufuku kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya kilomita 60
kutoka kwenye chanzo.
"Marufuku wafugaji kuingiza ng'ombe ndani ya
vyanzo vya maji na badala yake utafutwe utaratibu wa kuwachimbia mabwawa
pembeni. Pia wakulima nao wazuiwe kulima ndani ya vyanzo vya maji. Lazima
tushirikiane kulinda vyanzo vyetu," amesema.
Awali, Mhandisi Seif alisema kituo hicho cha Mtera
kinazalisha megawati 80 kwa siku ambazo zinaingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Alisema bwawa hili kwa sasa lina maji ya kutosha kuzalisha umeme hadi msimu
ujao wa mvua.
Mhandisi hiyo alisema bwawa hilo linategemea kupata
maji kutoka mto Ruaha Mkuu, mto Ruaha Mdogo na Vyanzo vyote hivyo vinaathiriwa
na shughuli za kibidamu ambapo watu wanalima na kuingiza mifugo.
Baada ya kutoka kituoni hapo Waziri Mkuu
alitembelea shamba la Igingilanyi ambalo ni moja kati ya mashamba matatu ya
kufugia ng’ombe yanayomilikiwa na kiwanda cha kuzalisha bidhaa za maziwa ya
Asas kilichoko mkoani Iringa.
Akiwa shambani hapo Waziri Mkuu aliwaagiza
wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia vizuri mgawanyo
wa ardhi ndani ya halmashauri zao pamoja na kusimamia mipaka kati ya wilaya na
wilaya.
“Wekeni mipango bora ya matumizi ya ardhi. Pimeni
ardhi na mgawe hati ili kumaliza migogoro ya ardhi hata kwa waliopewa mashamba
makubwa nao wapimiwe na ardhi yao na wapewe hati kwa mujibu wa muda uliowekwa
kisheria,” amesema.
Pia aliwataka Maofisa Mifugo kuongeza kasi ya
kutambua mifugo iliyoko kwenye maeneo yao na kuiwekea alama ili kuzuia uhamiaji
holela wa mifugo kwa lengo la kuzuia migogoro kati ya wafugaji na wakulima.
Kwa upande wake mmoja wa Wakurugenzi wa kiwanda cha
Asas, Bw. Fuad Abri alisema kiwanda hicho kina mashamba matatu yenye jumla ya
ekari 2,000 na ng’ombe 1,010 kati ya hao 350 hukamuliwa maziwa na kutoa wastani
wa lita 5,000 kwa siku.
Alisema katika mashamba hayo wameajiri wafanyakazi
175 na wamefanikiwa kutumia njia ya uhamilishaji (Artificial Insemination)
katika mashamba yote na njia hiyo inawasaidia kuchagua jinsia ya ng’ombe
wanayohitaji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMIS, JANUARI 19, 2017.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MARUFUKU KULIMA, KUINGIZA MIFUGO NDANI YA VYANZO VYA MAJI-MAJALIWA. ”
Post a Comment