Tuesday, March 18, 2014

IDARA YA MAJI WILAYA YA MAKETE YAJIPANGA KUTOA MAJI MAKETE MJINI KWA ASILIMIA 100 IFIKAPO MEI MWAKA HUU.




Idara ya maji wilayani Makete mkoani Njombe imejipanga kuhakikisha wakazi wa Makete mjini watapata maji kwa asilimia mia moja ifikapo Mei mwaka huu

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa mamlaka ya maji Makete mjini Bw. Yonasi Ndomba wakati akizungumza na mtandao huu katika wiki hii ya kuelekea kilele cha siku ya Maji duniani ambacho kwa mkoa wa Njombe kitaadhimishwa katika wilaya ya Makete katika viwanja vya mabehewani

Bw. Ndomba amesema kwa sasa ni asilimia 4 tu ya wakazi wa Makete mjini hawapati maji saa 24, hivyo kutokana na mikakati wanayeoendelea kuitekeleza kwa sasa, wanaimani hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu maji makete mjini yatapatikana kwa asilimia mia moja

Akizungumzia kilele cha wiki ya maji, amesema kimkoa maadhimisho yatafanyika wilayani hapa na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa mkuu wa mkoa wa Njombe Kapteni mstaafu Aseri Msangi, ambapo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo

Mkuu wa mkoa anatarajiwa kuweka jiwe la msingi ujenzi wa tanki la maji lililopo Mwongolo, Makete mjini pamoja na mkutano wa hadhara utakaofanyika katika viwanja vya mabehewani pamoja na burudani mbalimbali kutoka kwenye vikundi vya sanaa vilivyopo wilayani hapo

Kwa upande wake Kaimu mhandisi wa maji wilaya ya Makete Bw. Nahom Tweve ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuchunga mifugo kwenye vyanzo vya maji kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha maji kuzidi kupungua wilayani hapo, hivyo adha ya maji itazidi kuongezeka badala ya kupungua

Amesema kwa kuwa sheria zipo, yeyote atakayekamatwa na serikali akiharibu vyanzo vya maji atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo

"Miaka 30 iliyopita ndani ya wilaya hii kuna mito ilikuwa huwezi kuvuka kutokana na wingi wa maji, wapo wazee waliokuwepo enzi hizo watakuwa ni mashaidi, lakini kwa sasa mito hiyo unajivukia biala wasiwasi kwa kuwa maji yamepungua sana" amesema Tweve

Kaimu huyo amesema ni lazima kila mmoja wetu atunze vyanzo vya maji kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo, kwa kuacha kuchunga mifugo kwenye vyanzo vya maji, kupanda miti ambayo ni rafiki na vyanzo vya maji pamoja na kuacha uharibifu wowote ule kuhusu vyanzo vya maji

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni "uhakika wa maji na nishati"

0 Responses to “IDARA YA MAJI WILAYA YA MAKETE YAJIPANGA KUTOA MAJI MAKETE MJINI KWA ASILIMIA 100 IFIKAPO MEI MWAKA HUU.”

Post a Comment

More to Read