Monday, March 31, 2014

RAZA: TUACHE UTOTO TUJADILI KATIBA.




Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mohamed Raza ametaka wajumbe wenzake kuheshimiana bila kujali wingi au uchache wa wajumbe kwenye makundi yao, kama kweli wana dhamira ya dhati ya kutunga Katiba.

Akizungumza na gazeti hili, Raza alisema mwenendo wa Bunge siyo mzuri na hauleti picha nzuri kwa mamia ya wananchi ambao wanategemea wapatiwe Katiba bora itakayoondoa tatizo yao.

“Tupo hapa tunalipwa kwa siku Sh.300,000 na tunajua huku nyuma kuna maelfu ya wananchi wetu hawana hata Sh.1000 ya chakula, halafu tunakaa hapa tunafanya vurugu na kuacha kusikilizana hata katika hoja za msingi? Nadhani hatuwatendei haki wananchi,” alisema Raza.

Amesema hakuna asiyejua matatizo ya wananchi. Kinachotakiwa sasa ni kukaa na kuanza kupitia Rasimu ya Katiba, hasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba kuiwasilisha bungeni.

“Hakuna ambaye alizaliwa na mama yake na kuelezwa ipo siku atashiriki kuandika Katiba ya mamilioni ya wananchi wa Tanzania. Sasa hii ni fursa nzuri kwetu sote kukaa na kutafakari matatizo yetu na kuyapatia ufumbuzi katika katiba hii mpya,” alisema Raza.
Aidha amesema ni muhimu kujadili Rasimu ya Katiba katika muktadha wa kiuchumi ili kuhakikisha inakwenda kwa wananchi na kukubalika na siyo kutanguliza masilahi ya kisiasa au makundi wanayotoka wajumbe.

0 Responses to “RAZA: TUACHE UTOTO TUJADILI KATIBA.”

Post a Comment

More to Read