Friday, March 28, 2014

SAMWELI SITTA AWEKWA MTEGONI.




Suala la ama kutumia kura ya siri au ya wazi kuamua ibara za Rasimu ya Katiba jana liliuteka upya mjadala wa Kanuni za Bunge la Katiba, huku ikielezwa kuwa limewekwa kama mtego kwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta katika kuwania urais.

Sitta ni mmoja wa wanasiasa wanaotajwa kuwa katika kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu ujao kupitia CCM, huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mahasimu wake kisiasa ndani ya chama hicho.

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Godbless Lema alimtaka Sitta kuwa makini na maelekezo aliyodai mwenyekiti huyo anapewa katika uendeshaji wa Bunge na kudai pia kuwa, kuna kundi la watu wanaotaka urais katika Uchaguzi Mkuu 2015 wanaotaka kumkwamisha.

Akichangia hoja ya mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni yaliyotaka kupitishwa mifumo miwili ya kura kwa wazi na siri, Lema ambaye ni Mbunge wa Arusha alisema kwa mazingira ambayo yanaendelea, Sitta anapaswa kuwa makini na watu wanaompatia maelekezo wakitaka aonekane hafai baadaye.

“Ni vyema ukawa makini na mapendekezo unayoletewa kwa sababu hao wote pamoja na wanachama wa chama chako wanajua kama utaliongoza vizuri Bunge hili, basi unaweza ukapata tiketi ya kugombea urais 2015 ndani ya chama chako, lakini ukishindwa watakudhihaki kuwa umeshindwa, hivyo hutaweza kuliongoza taifa,” alisema Lema huku Sitta aliyeonekana awali akitabasamu, alibadilika na kumtazama mbunge huyo kwa umakini.

Lema alisema miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM na kamati nyingine za Bunge hilo, kuna watu ambao wanataka kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Katika mjadala huo, ilionekana wazi kuwa wajumbe bado wamegawanyika pande mbili – CCM wakionekana kuunga mkono kura ya wazi na upande wa upinzani wakipigia chapuo kura ya siri.
Miongoni mwa waliopigia debe kura ya siri ni John Mnyika aliyesema suala la upigaji kura ni la kikatiba ili kuhakikisha kila mjumbe anapiga kura yake bila kushurutishwa, kushinikizwa wala kupokea maelekezo kutoka kwa mtu au chombo chochote.

Wajumbe hao walikuwa wanajadili mapendekezo yaliyowasilishwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, Pandu Ameir Kificho, baada ya juzi kuzua mvutano uliosababisha Bunge hilo kuvunjika ili kusubiri maridhiano ya pande zinazopingana.

0 Responses to “SAMWELI SITTA AWEKWA MTEGONI.”

Post a Comment

More to Read