Tuesday, March 18, 2014
SERIKALI BADO HAIJATOA BILIONI 143 KWA AJILI YA UJENZI WA DARAJA LA KIGAMBONI.
Do you like this story?
Serikali
imeingia kwenye lawama ikidaiwa kukwamisha kasi ya ujenzi wa Daraja la
Kigamboni kutokana na kushindwa kutoa Sh.143.5 bilioni sawa na asilimia 40 ya
fedha za mradi huo hadi kukamilika.
Lawama
hizo zimekuja ikiwa miezi 15 imebaki kabla ya muda uliopangwa ujenzi huo
kukamilika Juni mwakani.
Kwa
upande wake, Serikali imesema haina taarifa ya kusuasua kwa kasi ya ujenzi na
kwamba suala la utoaji wa asilimia 40 litatekelezwa kulingana na taratibu.
Mmoja
wa wafanyakazi waandamizi wa mradi huo, ambaye hakutaka jina lake kuandikwa
kwenye gazeti, alisema kuwa kasi ya ujenzi imepungua kutokana na fedha kidogo
zinazotolewa kwa ajili ya uendelezaji.
"Kuna
kazi hazijafanyika hivi sasa na zingine zimesimama kabisa," alisema.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge amesema hawajapokea
malalamiko yoyote kutoka kwa makandarasi kuhusu suala la fedha kuchelewa kutoka
serikalini.
"Suala
la fedha kuchelewa ni 'logistic' za Serikali na siyo hoja ya msingi sana kama
daraja linaendelea kujengwa na hakuna kazi zilizosimama," alisema.
Lwenge
amesema kuwa fedha ambazo ni sehemu ya mchango wa Serikali zitapatikana na kuna
kila dalili ujenzi ukakamilika kabla ya muda uliopangwa.
Mkuu
wa Idara ya Uhusiano Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eunice Chiume
alikiri kuwa fedha kutoka serikalini hazijatolewa mpaka sasa.
Amesema
fedha za Serikali zinapaswa kutumika kujenga barabara zinazounganisha daraja
hilo na maeneo ya Kigamboni kwa upande mmoja na Barabara ya Shimo la Udongo.
"Fedha
za Serikali ni kwa ajili ya ujenzi wa barabara zenye urefu kilomita 1.5 kila
upande kwa kiwango cha lami, lakini hadi sasa hatufahamu ujenzi wa barabara
hizo utaanza lini," amesema.
Aliongeza:
"Halitakuwa jambo zuri daraja kukamilika bila barabara hizo kujengwa,
kwani hali hiyo inaweza kuchangia msongamano usio wa lazima. Kwanza siyo vizuri
kwa daraja lenyewe kuwa na lami, kisha likaunganishwa na barabara za
vumbi."
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SERIKALI BADO HAIJATOA BILIONI 143 KWA AJILI YA UJENZI WA DARAJA LA KIGAMBONI.”
Post a Comment