Thursday, April 24, 2014
POSHO YALAINISHA MSIMAMO WA UKAWA, BAADHI WARUDI KUDAI POSHO ZAO BUNGENI.
Do you like this story?
UTAMU wa posho katika Bunge Maalumu la
Katiba, umeathiri siasa za baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo waliojiundia kundi
la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wajumbe hao waliondoka bungeni kwa
mbwembwe wakisusia vikao vya Bunge hilo na kudai hawarudi ng’o, lakini jana
baadhi yao walirejea kinyemela bungeni na kwenda moja kwa moja Ofisi ya Katibu
wa Bunge Maalumu, kudai posho za vikao ambavyo hawajashiriki.
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta
juzi mchana alitangaza bungeni kuwa, amepata taarifa kuwa wajumbe wa Ukawa
wamerudi lakini si katika vikao bali wameonekana kwa Mhasibu kuchukua posho.
“Kuhusu hilo la Ukawa kurudi, taarifa
zilizonifikia hivi punde zinaeleza kuwa wamerudi, lakini wameenda kwa Mhasibu
kuchukua posho,” alisema Sitta na kusababisha wajumbe waliokuwepo ndani ya
Bunge hilo kucheka.
Wanyang’anywa tonge
Baada ya Sitta kueleza hivyo,
alimkaribisha Mjumbe Adam Malima, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, kutoa
taarifa kuhusu hatua hiyo ya Ukawa kurudi kuchukua posho.
Malima alisema utaratibu wa fedha
zinazolipwa na Serikali ni kwa wajumbe wanaokuja katika kazi za Bunge hilo na
kuongeza kuwa, Serikali haipo tayari kuwalipa watu ujira ambao hawajaufanyia
kazi.
“Tumezungumza na Katibu wa Bunge na
kukubaliana kwamba, wote wasio na mahudhurio malipo yao yasitishwe kwanza,
hawawezi kuchukua fedha wakati hawajafanya kazi, hili tunaiachia Kamati ya
Uongozi ya Bunge Maalumu,” alisema Malima.
Baada ya Malima kumaliza kutoa taarifa
hiyo, Sitta alisisitiza kuwa, wajumbe hao hawawezi kuchukua fedha kwa kugoma
kufanya kazi iliyowapeleka Dodoma.
Washitukiwa
Akizungumza na Habari leo jana, Katibu
wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hamad, alikiri kuwa baadhi ya wajumbe wa Ukawa
walirudi kuchukua posho lakini hakuwataja majina.
Alisema juzi walitangaza wajumbe wajaze
fomu kwa ajili ya malipo yao na inavyoonekana, baadhi ya wajumbe wa Ukawa, kwa
kujua wahasibu hawawafahamu vizuri kama wapo bungeni ama ni miongoni mwa
walioondoka, walichukua fomu na kujaza kuchukua posho.
“Kabla ya malipo yoyote, utaratibu wetu
ni lazima wajumbe wajaze fomu za malipo, jana (juzi) tulitangaza wajumbe wajaze
fomu kwa ajili ya malipo, Ukawa nao waliingia na kuna fomu walijaza, nimechukua
orodha ya mahudhurio ili kujua waliohudhuria.
Hata ya kujikimu?
“Nimeagiza asubuhi hii fomu zote
niletewe, ambaye hakuwa ndani hata kama si Ukawa ataeleza alikuwa wapi, kama
hakuwa ndani hatutamlipa mpaka Mwenyekiti (Sitta) aidhinishe kwamba mhusika
alikuwa na dharura ya muhimu akiwa Dodoma ndio atalipwa posho ya kujikimu
lakini si ya kikao,” alisema Katibu huyo.
Alisema mjumbe yeyote atakayelipwa
posho ya kikao ya Sh 70,000 ni aliyehudhuria kikao na kujaza fomu lakini posho
ya kujikimu ya Sh 230,000, italipwa kwa mjumbe aliyefika Dodoma kwa ajili ya
Bunge hata kama alipata dharura ya kutohudhuria vikao kadhaa.
Kwa mujibu wa Yahaya, posho zinazolipwa
ni za kuanzia Aprili 19 mwaka huu hadi Aprili 26 na kwamba za kuanzia Aprili 18
kurudi nyuma, zote zilishalipwa.
Hata hivyo, alifafanua kuwa posho ya
kujikimu pamoja na kwamba hulipwa mjumbe akiwasili Dodoma, wapo wajumbe ambao
hawajalipwa kutokana na kukosekana ufafanuzi wa dharura zao lakini maelezo ya
Sitta ya uthibitisho yakitolewa, watalipwa.
Kamati ya Uongozi
Akizungumzia kuhusu uamuzi wa Kamati ya
Uongozi ya Bunge Maalumu iliyokuwa ikae Alhamisi iliyopita kujadili hatma ya
posho za wajumbe wa Ukawa, Yahaya alisema kikao hicho hakikufanyika.
Alifafanua kwamba sababu ya kutofanyika
kikao hicho ni kutokuwa na taarifa kamili kwa kuwa Sitta aliomba kwenda
Zanzibar, kukutana na baadhi ya viongozi wakiwemo wa Ukawa kutafuta suluhu.
Katibu alisema Kamati ya Uongozi
inaweza kukutana muda wowote kuanzia sasa kwa kuwa Sitta amesharejea bungeni.
Sitta alikwenda Zanzibar Jumatatu wiki
hii, ambapo pamoja na kukutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Seif Sharif Hamad, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa
Chama cha Wananchi- CUF, pia alikutana na Rais wa SMZ, Dk Ali Mohamed Shein na
Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
>>Habari leo
>>Habari leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ POSHO YALAINISHA MSIMAMO WA UKAWA, BAADHI WARUDI KUDAI POSHO ZAO BUNGENI.”
Post a Comment