Friday, June 20, 2014
SABASABA 2014 KUUNGANISHA UZALISHAJI NA MASOKO.
Do you like this story?
Maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar-es-salaam (38th DITF)
yanatarajia kuanza tarehe 28 mwezi huu na kufikia kilele chake
tarehe 8 Julai 2014 katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu J.K.
Nyerere, barabara ya kilwa, jijini Dar-es-salaam.
Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade
Bibi. Jacqueline Mneney Maleko imeeleza kuwa
maonesho ya mwaka huu yataongozwa na kauli mbiu isemayo
“Tunaunganisha Uzalishaji na Masoko”
Amesema kuwa Kauli Mbiu hiyo imechaguliwa kutumika kuonesha uhusiano
uliopo kati ya Uzalishaji na Masoko na umuhimu wa mnyororo wa
uzalishaji ambao ndio chimbuko la upatikanaji wa Bidhaa bora zenye ushindani
katika soko.
Bibi. Maleko amesema kuwa mwaka huu TanTrade imetenga eneo kubwa zaidi
kwa ajili ya Wazalishaji wa ndani ya nchi na kubainisha maeneo yatakayotumiwa
na wazalishaji hao kuwa ni jengo namba C.19 na eneo la wazi lililo nyuma ya
ofisi za Mkurugenzi wa Utafiti, Mipango na Uwezeshaji kwa ajili ya bidhaa za
kilimo na bidhaa zinazotengenezwa Tanzania.
Kuhusu ushiriki wa mataifa mengine katika maonesho hayo amefafanua kuwa
tayari nchi 31 zimethibitisha kushiriki maonesho hayo zikiwemo Afrika
Kusini,Czech Republic, China, Ghana, Indonesia, India, Iran, Finland, Ugiriki,
Italia, Japan, Jordan, Kenya, Korea ya Kusini, Malaysia, Marekani, Misri, na
Ujerumani.
Nchi zingine ni pamoja na Nigeria, Pakstani, Rwanda, Saudi Arabia,
Singapore, Sudani, Syria, Uganda, Uingereza, Burundi, Sweden, Vietnam na
Zimbabwe.
Aidha, amefafanua kuwa makampuni ya nje 490 yamethibitisha kushiriki
katika maonesho hayo huku Wizara na Taasisi za Serikali zilizothibitisha
kushiriki maonesho hayo zikifikia 61.
Kwa upande wa Mikoa amesema tayari mikoa 10 imethibitisha kushiriki
ikiwemo, Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Mbeya, Pwani, Kigoma, Kagera, Geita, Mara,
Manyara na Ruvuma. Jumla ya Washiriki waliothibitisha kushiriki kutoka ndani ya
nchi ni 1700.
Kuhusu kiingilio wakati wa maonesho hayo amesema watu wazima
walipia Shilingi 2,500 na watoto ni 500 kila siku kwa siku zote za
maonesho isipokuwa tarehe 7 Julai,2014 ambapo ada itakuwa Shs. 3,000/= kwa watu
wazima na watoto ni Shs.1000/=
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SABASABA 2014 KUUNGANISHA UZALISHAJI NA MASOKO.”
Post a Comment