Thursday, October 30, 2014
DAR ES SALAAM ZANZIBAR KUUNGANISHWA KWA DARAJA
Do you like this story?
BAADA ya ndoto ya
kuziunganisha pande mbili za katikati ya Jiji la Dar es Salaam na Kigamboni kwa
daraja lenye umbali wa meta 680, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)
linaangalia uwezekano wa kujenga daraja la kihistoria zaidi litakalounganisha
Dar es Salaam na Zanzibar.
Kwa sasa, uongozi wa
shirika hilo upo katika mazungumzo na wataalamu mbalimbali ili kuangalia
uwezekano wa kujenga daraja hilo katika bandari ya Dar es Salaam kwa upande wa
Tanzania Bara na Unguja, kwa upande wa Zanzibar.
Umbali kati ya Dar es
Salaam na Zanzibar ni kilometa 73.43, sawa na maili 45.62 hivyo kuwapo kwa
mradi huo ni jambo linalowezekana, kwani kuna madaraja marefu zaidi duniani
yanayounganisha upande mmoja wa bahari na mwingine.
Kwa sasa, daraja refu
kabisa duniani ni lile la Danyang–Kunshan lililopo China ambalo lina umbali wa
kilometa 165, sawa na maili 102.4. Daraja hilo lilifunguliwa Juni mwaka 2011.
Hayo yameelezwa na
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhan Dau wakati alipokuwa akijibu swali la
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda
ambaye alitaka kufahamu kama kuna matarajio ya kujenga daraja kubwa zaidi,
ikiwezekana la kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Alisema wapo katika
mazungumzo na wataalamu mbalimbali ambapo mazungumzo hayo yakienda sawa, ujenzi
wa daraja hilo huenda isiwe ndoto, bali ukweli.
"Hilo wazo lipo
mheshimiwa na tayari tumeshaanza mazungumzo ya awali, kwa hiyo hilo wazo lipo
na sisi tulilifikiria," alisema Dk Dau.
Kamati hiyo ilifanya
ziara katika miradi mikubwa mitatu ya shirika hilo ambayo ni daraja la
Kigamboni, ujenzi wa nyumba za Mtoni Kijichi na 'Dege Eco village' ambao una
nyumba zaidi ya 7,000.
Akizungumza wakati wa
kuhitimisha ziara hiyo, Mtanda alisema, kamati yake imeridhishwa na miradi hiyo
ya NSSF ambayo inaendelea huku akitaka kuongezwa kwa kasi ili watanzania waanze
kunufaika na miradi hiyo.
"Muangalie na
hilo la ujenzi wa daraja la kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar na mradi wa
makazi bora na salama ambao utaweza kubadili taswira ya Jiji la Dar es
salaam," alisema.
Alisema kamati yake
isingependa kuona changamoto zozote ambazo zinaweza kukwamisha miradi hiyo na
kwamba serikali kupitia Wizara ya Ujenzi itaangalia namna ya kuunganisha
miundombinu karibu na miradi hiyo.
"Lakini pia
tumesikia kuwa serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi, tunashauri serikali
kuilipa mifuko hii ili kuifanya kuwa na nguvu
na kuweza kuleta
maendeleo," alisisitiza Mtanda.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “DAR ES SALAAM ZANZIBAR KUUNGANISHWA KWA DARAJA ”
Post a Comment