Tuesday, October 21, 2014
WALIMU 422 WAFUTWA KAZI, WAMO WALIOFANYA MAPENZI NA WANAFUNZI WAO
Do you like this story?
Jumla ya walimu 422 wamefutwa kazi kwa makosa mbalimbali ikiwemo
kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi kwa kipindi cha mwaka
2013/2014.
kiwango cha walimu wanaokwenda kinyume na maadili na kufutwa kazi
kimeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo katika kipindi cha mwaka
2013/2014 walimu 422 wamefutwa katika maeneo mbalimbali nchini, wakiwemo
watatu kwa kubainika kujihusisha kimapenzi na wanafunzi na wawili kwa
kuwaonesha wanafunzi mitihan, ikilinganishwa na walimu 278 mwaka 2012/2013.
Katibu msaidizi wa idara ya utumishi wa walimu, Christina Hape, amesema
hayo mjini Morogoro, na kubainisha kuwa mwaka 2012/2013 walifutwa kazi asilimia
98 ya walimu 151 ambao mashauri yao yalipelekwa katika idara hiyo kwa
mapendekezo ya kufutwa kazi, ambapo amesema sababu kubwa ya walimu kufutwa kazi
ni utoro unaotokana na wengi kwenda kujiendeleza kielimu bila ruhusa ya
mwajiri.
Amesema makosa makubwa yakiwemo ya mwalimu kubainika kuwa na
mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi ama kuonesha mitihani, husababisha mwalimu
kufukuzwa kazi sambamba na utumishi serikalini na binafsi, huku makosa
mengine kama utoro, mwalimu akifukuzwa kazi na kuachiwa utumishi wake.
Naye kaimu katibu mkuu wa tume ya utumishi wa umma, ambaye pia ni naibu
katibu idara ya utumishi, Rose Elipenda, ametoa wito kwa waajiri kusimamia
vyema utumishi wa watumishi, kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za kazi
na kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao ya kazi kabla ya
kufikisha mashauri yao katika mamlaka za juu kwa maamuzi zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya idara ya utumishi wa walimu, watumishi hao
wanapaswa kuhakikisha wanatii mamlaka za kisheria zilizowaweka katika nafasi
zao sambamba na kuzingatia kuwa ualimu sio taaluma pekee bali pia suala
zima la maadili kwani wakimpotosha mtoto wanayeaminiwa kumjenga kiakili, ni
kupotosha taifa zima.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WALIMU 422 WAFUTWA KAZI, WAMO WALIOFANYA MAPENZI NA WANAFUNZI WAO ”
Post a Comment