Wednesday, April 15, 2015
MKURUGENZI SUMATRA ATOA TAMKO KUHUSU NAULI ZA MABASI NA DARADALA.
Do you like this story?
MKURUGEZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti na
Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA)ametoa tamko kuhusiana na nauli elekezi
ya mabasi ya masafa marefu na mijini.
Akizungumza na wanahabari katika ofisi zao
jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi huyo Gilliad Ngewe alisema mwishoni mwa mwaka
2014, mafuta yatumikayo katika vyombo vya usafiri wa abiria nchini yalianza
kushuka hivyo mamlaka ya udhibiti usafiri wa nchi kavu na majini
(Sumatra)ilikuwa ikipokea wito wa kupitia upya viwango vya juu vya nauli.
Alisema kuwa viwango hivyo vilikuwa vimewekwa
na mamlaka Aprili 2013 na hivyo SUMATRA ikaamua kuandaa mikutano ya wadau kwa
lengo la kukusanya maoni kuhusu haja ya kurekebisha viwango vya nauli zilizopo.
Aidha alisema kuwa mnamo Machi mwaka huu
baraza la ushauri la watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na Sumatra
liliwasilisha kwa Mamlaka ya Udhibiti na Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA) maombi ya kushusha nauli za mabasi ya masafa marefu na mijini ambapo
baraza liliainisha sababu za kuomba punguzo hilo kuwa ni kutokana na kushuka
kwa bei za mafuta na kodi ya forodha kutoka asilimia 25 hadi punguzo la
asilimia 10 kuanzia Julai 2014.
Ngewe alieleza namna walivyokubaliana na Bodi
baada ya kutafakari viwango vilivyotokana na ukokotoaji uliozingatia masuala
muhimu ili kukidhi matakwa ya watumiaji wa vyombo vya usafiri hivyo bodi
iliridhia viwango vya nauli vilivyopo kuendelea kutumika kama kawaida kutokana
na sababu iliyopelekea kubaki hapo ikiwa mojawapo ni usumbufu wa kurudisha
chenji kutoka 376.77 iliyokuwa imekokotolewa ikiwa na punguzo la asilimia 5.8
hivyo nauli kubakia sh.400 za daladala.
Vilevile alieleza namna Bodi ilivyoamua kuwa
nauli za mabasi ya hadhi ya juu (Luxury bus) kuwa hazitadhibitiwa ili kuchochea
ubunifu katika utoaji huduma na ushindani kati ya huduma za barabara na njia
nyinginezo za usafiri na katika viwango hivyo vipya vinapatikana katika tovuti
ya mamlaka ambayo ni www.sumatra.go.tz.
Katika ufafanuzi wa viwango vipya vya mabasi
ya masafa marefu, Ngewe alisema kuwa kutakuwa na jumla ya madaraja manne ambayo
ni daraja la kawaida la chini barabara ya Lami 36.89 ya sasa ikiwa viwango
vipya ni 34.00, punguzo ikiwa asilimia7.8, daraja la kawaida la chini barabara
ya vumbi vya sasa ni 46.11 vipya ikiwa ni 42.50 sawa na asilimia 7.8, daraja la
kawaida la juu 44.96 pamoja na daraja la kati la (Semi –Luxury bus) nauli ya
sasa 53.22 nauli mpya ikiwa ni 50.13 sawa na punguzo la asilimia 5.81.
Alihitimisha kwa kusema kuwa viwango hivyo
vya mabasi vinatarajia kuanza Aprili 30 mwaka huu na kuwaomba abiria wote kwa
ujumla kutoa taarifa kwa SUMATRA endapo watatozwa zaidi ya nauli elekezi
kuanzia siku hiyo kwa kupiga simu za bure ambazo ni 0800110019 au 0800110020.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MKURUGENZI SUMATRA ATOA TAMKO KUHUSU NAULI ZA MABASI NA DARADALA.”
Post a Comment