Wednesday, January 27, 2016
ANDREW CHENGE ACHAGULIWA KUWA MWENYEKITI WA BUNGE........ASEMA SUALA LA ESCROW LIKIRUDI BUNGENI ATAKAA PEMBENI.
Do you like this story?
MBUNGE wa
Bariadi, Andrew Chenge na wabunge wawili wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa na
Najma Giga, wamechaguliwa kuwa Wenyeviti wa Bunge kwa kipindi cha miaka miwili
na nusu.
Uchaguzi huo
ulifanyika jana baada ya majina yao kupendekezwa na Kamati ya Uongozi na
kuyawasilisha bungeni kwa ajili ya uchaguzi.
Katika uchaguzi
huo, uliotanguliwa na wabunge hao kujieleza mbele ya wenzao na kuulizwa
maswali, sakata la Tegeta Escrow liliibuka baada ya Chenge kujieleza.
“Katika
Bunge lililopita, chama chako na wabunge walikuwajibisha kwa kashfa ya Escrow,
je, siku ukiliongoza Bunge na hoja ikarudi ndani uko tayari kuisimamia,” Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema) alimuuliza Chenge.
Akijibu swali
hilo, Chenge alisema Bunge linaongozwa na Kanuni na itakapokuja mbele ya Bunge
au kwenye Kamati, ikaonekana kuna maslahi ama inamhusu mbunge, ni busara
kuzingatia kanuni nafasi hiyo ikaachwa mwingine aifanye shughuli za Bunge
zisiwe na makandokando ya aina yoyote.
“Naona
niishie hapo, ningeweza kusema zaidi ya hapo,” alisema Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kwa zaidi ya miaka 10 na pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la 10
kabla ya kujiuzulu kutokana na sakata la Tegeta Escrow.
Awali
akijieleza Chenge ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria
Ndogo, alisema “napenda niliahidi Bunge na Watanzania kwa ujumla, kwamba hii
ni dhamana nzito ya kumsaidia Spika na Naibu.
“Lakini
niwahakikishie nitatekeleza jukumu hilo kwa uadilifu, na kwa uaminifu ili
nitende haki inayoonekana na bila chuki, wala upendeleo wowote kwa faida ya
kujenga misingi bora ya Bunge hili lakini pia kwa kuwatumikia Watanzania wote,” alisema.
Kuhusu swali la
Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM) aliyetaka kufahamu ni namna gani Chenge
atadhibiti matumizi ya lugha ya kuudhi au kudhalilisha wengine, Chenge alisema
Kanuni za Bunge kama zilivyo sheria za nchi, zinakata pande zote kama ilivyo
msumeno.
Alisema
ikithibitika kwamba mbunge amekiuka kanuni, kiti kitazingatia baada ya kupima
kauli na maelezo aliyotoa bungeni.
“Baada
ya kupima, tuhakikishe kwamba tunayosema humu bungeni yawe ya kweli, kweli tupu
yasiwe ya uongo,” alisisitiza.
Mwanjelwa
ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Mbeya, katika kujieleza mbele ya
wabunge, aliomba wamwamini na kuahidi kuwatumikia bila kujali itikadi kwa faida
ya wananchi wote.
Mwanjelwa
alikiri kwamba Bunge hili lina changamoto nyingi, lakini atakachozingatia ni
utaifa kwanza.
Najma, ambaye
kitaaluma ni Mwanasheria, aliahidi kuwa msaada mkubwa kwa Spika. Aliahidi kuwa
atahakikisha anaweka maslahi ya taifa mbele kwa kutoa haki sawa kwa wabunge
wote bila kujali vyama vyao.
Spika wa Bunge,
Job Ndugai alihoji kwa pamoja wanaoafiki mapendekezo ya Kamati ya Uongozi,
ndipo wabunge walio wengi wakaridhia Chenge, Mwanjelwa na Najma wawe wenyeviti.
Wenyeviti wa Bunge hufanya kazi wakati ambao Spika au Naibu Spika wakiwa hawapo
bungeni.
Katika Bunge la
10, wenyeviti walikuwa Mussa Azzan Zungu, Kidawa Himid Saleh, Lediana
Mng’ong’o, Muhammed Seif Khatib, Sylvester Masele na Jenista Mhagama.
Kwa mujibu wa
Ndugai, Kamati yau Uongozi imejiwekea utaratibu wa kupendekeza majina na
ilipokutana chini ya uenyekiti wa spika, iliamua kuwapendekeza wabunge hao
watatu ambao wote ni kutoka CCM.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ ANDREW CHENGE ACHAGULIWA KUWA MWENYEKITI WA BUNGE........ASEMA SUALA LA ESCROW LIKIRUDI BUNGENI ATAKAA PEMBENI.”
Post a Comment