Friday, June 17, 2016
TANZANIA KUANZA KUTUMIA KISWAHILI KATIKA MIKUTANO YOTE YA KIMATAIFA.
Do you like this story?
TANZANIA
inatarajiwa kuanza kutumia Kiswahili katika mikutano yote ya kimataifa
itakayowakilishwa na viongozi wake baada ya serikali kukamilisha kutuma
wataalamu watakaotafsiri lugha hiyo kwa watumiaji wa lugha nyingine duniani.
Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa alisema hayo jana katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo
kwa Waziri Mkuu, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu
Vulu (CCM).
Vulu
katika swali lake alihoji namna serikali inavyoenzi lugha ya Kiswahili ambayo
ilitumika na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuunganisha Taifa na
inatumiaje fursa ya kutumika kwa lugha hiyo kimataifa, kuwa ajira kwa
Watanzania.
Akifafanua
jibu lake, Majaliwa alisema tayari serikali ilishaamua Kiswahili kuwa lugha
rasmi ya kutumika serikalini na hata bungeni na sasa lugha hiyo imekua zaidi na
kuwa moja ya lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kwa mujibu
wa Majaliwa, tayari duniani kote vyuo vikuu vimeanza kufundisha Kiswahili, hali
iliyosababisha kuongezeka kwa mahitaji ya walimu wa kufundisha lugha hiyo
kutoka Tanzania.
Kutokana
na uhitaji huo, Majaliwa alisema vyuo vikuu karibu vyote nchini, vinafundisha
walimu wa lugha hiyo kwa ajili ya kukidhi mahitaji hayo ya kimataifa, lakini
pia serikali inajiandaa kupeleka wataalamu wa kutafsiri Kiswahili kwenda katika
nchi mbalimbali.
Alisema
lengo la serikali kupeleka wataalamu hao katika nchi mbalimbali ni kuwezesha
viongozi kutoka Tanzania wanapokwenda katika mikutano ya kimataifa, watumie
Kiswahili na wataalamu hao watoe tafsiri kwenda kwenye lugha nyingine za
kimataifa.
Alisema
kwa sasa Tanzania imeshapeleka walimu wa lugha hiyo Burundi, Rwanda, Uingereza
na Ufaransa ambako wanafundisha lugha hiyo na kati ya lugha kubwa za kimataifa,
Kiswahili kama si lugha ya sita ni ya nane.
Naye
Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima (CCM), alimtaka Waziri Mkuu kuangalia
uwezekano wa kuruhusu wabunge kuwa wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama za
wilaya na mikoa.
Akijibu
ombi hilo, alisema wajumbe wa kamati hizo katika wilaya, mikoa na kitaifa,
wameainishwa na Sheria ya Usalama wa Taifa kuwa ni wakuu wa vyombo vya ulinzi
na usalama, ambao ni tofauti na mbunge ambaye ni mwakilishi wa wananchi
kisiasa.
Alisema
majukumu yao ni kuangalia hali ya usalama kwa undani, lakini sheria hiyo
haijamzuia mbunge au mwananchi yeyote, kwenda kutoa taarifa kama ilivyotokea
katika mauaji ya hivri karibuni, ambapo kamati hizo kutokana na ushirikiano
kutoka kwa wananchi, wahusika wameanza kukamatwa mmoja baada ya mwingine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ TANZANIA KUANZA KUTUMIA KISWAHILI KATIKA MIKUTANO YOTE YA KIMATAIFA.”
Post a Comment