Sunday, June 5, 2016

UKAWA WAMKIMBIA NAIBU SPIKA NJE YA BUNGE




MSIMAMO wa wabunge wa upinzani wa kususia kushiriki vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson umechukua sura mpya.

Jana wabunge hao walitoka ndani ya ukumbi wa Pius Msekwa uliopo bungeni mjini Dodoma  baada ya kiongozi huyo kupewa nafasi ya kufungua semina ya wabunge kuhusu Malengo Endelevu ya Dunia.
 
Semina hiyo ilikuwa imeandaliwa na Umoja wa Mataifa kupitia mpango wake wa kufanya kazi pamoja (Delivering as One).

Wabunge wa upinzani wanaotoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walitoka ndani ya ukumbi huyo baada ya Naibu Spika huyo kupewa nafasi ya kufungua semina hiyo iliyoanza saa nne asubuhi.

 
Wabunge hao walirejea ukumbini na kushiriki semina hiyo baada ya Dk. Ackson kumaliza kuwasilisha hotuba yake.
 
Kususa kwa wabunge hao jana kulikuja baada ya kuwa walikuwa wamesusa kuhudhuria vikao vya Bunge vilivyoongozwa na Dk. Ackson kwa siku nne mfululizo mpaka Ijumaa.
 
Kambi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikifanya hivyo dhidi ya Naibu Spika huyo tangu uongozi wa kambi hiyo utangaze kutokuwa na imani naye Jumatatu.
 
Tayari wabunge hao wamewasilisha hoja ya azimio la kutaka kumng'oa madarakani yenye sababu sita.
 
Jumanne iliyopita, kambi hiyo ilianza utaratibu huo wa kutoka kwenye ukumbi wa Bunge mara tu baada Naibu Spika kuingia.
 
Upinzani unachodai kutoridhishwa na uendeshwaji wa chombo hicho cha kutunga sheria chini ya Naibu Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani wa serikali.
 
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alitangaza Jumatatu kuwa upinzani hauna imani na Naibu Spika na hautakuwa tayari kushiriki vikao vinavyoongozwa na kiongozi huyo wa Bunge hadi pale "haki itakapopatikana".
 
Kutokana na msimamo huo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, aliuomba uongozi wa Bunge kutolipa mishahara na posho za wabunge wa kambi hiyo waliosusa Jumanne.
 
Hata hivyo, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, aliponda pendekezo hilo .
 
"Kama tuliacha posho ya Sh. milioni 30 za Bunge la Katiba, itakuwa hii ya vikao vya Bunge la Bajeti ambayo haifiki hata milioni tano?” Alihoji Mchungaji Msigwa.
 
"Hoja hapa si fedha, hoja ni misingi ya uendeshaji wa Bunge. 
 
"Hatuwezi kukubali kuburuzwa eti kwa sababu tunapewa posho."


0 Responses to “UKAWA WAMKIMBIA NAIBU SPIKA NJE YA BUNGE”

Post a Comment

More to Read