Sunday, June 5, 2016

WENYE SIMU FEKI KUPEWA MPYA BURE.




WAKATI Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikitarajia kuzima simu bandia ifikapo katikati ya mwezi, zimeibuka habari njema kwa watumiaji wa simu hizo feki nchini

Wale ambao simu zao zinatarajiwa kuzimwa siku 11 zijazo, sasa wamepata fursa ya kuendelea kuwapo katika ulimwengu wa teknolojia ya mawasiliano kwani watapatiwa simu mpya. Kampuni ya simu za mkononi Tigo, imetangaza ofa ya kuchukua simu feki kutoka kwa wateja na kuwapatia mpya bure.

Meneja wa Chapa ya Tigo, William Mpinga amesema kuwa ofa hiyo itawahusu watumiaji wote wa simu ambazo ni bandia. Alisema mradi huo unalenga kuwawezesha Watanzania kupata simu halisi kutokana na ukomo wa matumizi ya simu feki kuwa ni Juni 16. 

“Tunawataka wateja wetu kutembelea maduka ya Tigo ya huduma kwa wateja yaliyopo nchi nzima, kuhakiki simu zao na baada ya kuhakiki, wote wataobainika kuwa na simu feki watapata simu halisi aina ya Itel 2100," alisema Mpinga. Alisema watapata simu hizo bure watakaponunua kifurushi cha Sh. 22,000 ambacho kitawezesha kupata vifurushi vya miezi mitatu.

Akizungumzia mahali watakapozipeleka simu feki wanazozikusanya, mpinga alisema hatua zitafuata baada ya kuzikusanya na kwamba hawana lengo la kuziuza tena wala kuzitengeneza. Akizungumza na Nipashe, Meneja wa Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungi aliupongeza mpango huo na kusema unawapunguzia wananchi machungu. “Tigo au kampuni nyingine ina mamlaka ya kutoa ofa kama ambavyo imewapendeza kuwapunguzia machungu wateja wao, na kama promosheni nyingine zilivyo ili mradi hawatoi simu feki tena,” alisema.

Alisisitiza kuwa hakuna simu feki ambayo itaweza kufanya kazi tena baada ya Juni, na kwamba watumiaji wenye simu bandia waendelee kuzima simu zao kabla ya siku hiyo kufika. “Kama IMEI yako imeshasoma kuwa simu yako ni bandia kwa usalama wako izime na ondoa betri kwa sababu haitafanya kazi tena,” alisema Mungi.

Miezi sita iliyopita TCRA ilibainisha sababu za kuzima simu feki ni kutokana na kutokuwa na viwango vya ubora unaokubalika, lakini pia husababisha matatizo ya kiafya hasa kwenye ubongo kwa watumiaji.

0 Responses to “ WENYE SIMU FEKI KUPEWA MPYA BURE.”

Post a Comment

More to Read