Tuesday, August 16, 2016

JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LIMESEMA LIKO TAYARI KUTOA KIBALI KWA CHAMA CHOCHOTE CHA SIASA.




JESHI la polisi mkoani Mbeya limesema liko tayari kutoa kibali kwa chama chochote cha siasa kinachotaka  kufanya mikutano ikiwa kitafuata sheria na taratibu za nchi.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari katika Ofisi za Kituo kikubwa cha Polisi Mkoa wa Mbeya kuhusu matukio mbalimbali ya kiharifu yaliyotokea.

Amesema kuwa vibali hivyo vitatolewa kulingana na mazingira ya wakati husika kwa madai kuwa, hakuna utaratibu wa kufanya mikutano katika Wilaya zote kwa wakati mmoja.

Amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria, mikutano hiyo inahitaji ulinzi wa polisi kwa ajili ya kulinda amani,  hivyo akasema kuwa lazima vibali hivyo vizingatie hali ya wakati huo.

“Haiwezekani tukaruhusu maandamano katika Wilaya zote maana maandamano na mikutano hiyo inahitaji ulinzi wa Jeshi la Polisi, sasa tukiruhusu vitu kama hivyo tutashindwa kuweka ulinzi katika mikutano hiyo, kwa hiyo tutaangalia mtu atakayefuata taratibu ndiye atakayeruhusiwa na kupewa ulinzi,” alisema Kidavashari.

Amesema kuwa yeyote atakayeomba kibali kwa mujibu wa taratibu ndiye atakaye pewa ulinzi, lakini atakayekiuka atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Aliwataka wananchi kutokubali kurubuniwa na wanasiasa ili kushiriki katika maandamano yaliyokatazwa kwa madai kuwa watashughulikiwa na jeshi hilo kwa mujibu sheria zinavyotaka jeshi hilo kufanya.

Aliwataka kuwa na uhakika na mikutano wanayohudhuria endapo inakuwa imeruhusiwa ama la, ili wasijewakajikuta wanajiingiza katika matatizo.

Siku za hivi karibuni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilitangaza kuwa kufikia Septemba mosi mwaka huu kitafanya maandamano nchi nzima ili kupinga kile walichokiita udikteta ambayo waliyabatiza jina la Ukuta.

0 Responses to “JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LIMESEMA LIKO TAYARI KUTOA KIBALI KWA CHAMA CHOCHOTE CHA SIASA.”

Post a Comment

More to Read