Wednesday, August 17, 2016
MABASI YA MIKOANI KUGOMA JUMAPILI.
Do you like this story?
CHAMA cha
Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimesema kitasitisha huduma ya kusafirisha
abiria kwenda mikoa yote nchini Jumapili ili kufanya ukaguzi wa mabasi yake,
hatua ambayo itakuwa sawa na mgomo.
Aidha, Taboa
imesema inapinga uamuzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi
Kavu (Sumatra) kutangaza kuyafungia mabasi yote ya kampuni ya City Boy badala
ya moja ambalo lilisababisha ajali mkoani Singida hivi karibuni.
Julai 4, mabasi
mawili ya kampuni hiyo yaligongana uso kwa uso na kusababisha vifo vya watu
zaidi ya 30 wilayani Manyoni mkoani Singida.
Taboa imesema
pia itaipeleka serikali mahakamani kutokana na kufungiwa kwa mabasi hayo kwani
kwa mujibu wa sheria, aliyetakiwa kulifungia ni waziri mwenye dhamana na si
Sumatra kama ilivyofanyika.
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kumaliza kikao cha
dharura cha wamiliki wa mabasi ya mikoani, Katibu wa Taboa, Enea Mrutu, alisema
hawatakatisha tiketi kuanzia Jumapili ili kujipa muda wa kukagua mabasi yao
kama yana uwezo wa kufanya safari ama la.
"Tumeamua
kwa pamoja kuwa, kwa sababu tayari tumeshafanya 'booking' ya abiria, kuanzia
Agosti 21 mwaka huu, tuanze kufanya ukaguzi wa mabasi yetu kote nchini ili yale
ambayo hayana sifa yakae pembeni na yale yanayostahili kusafirisha abiria
yafanye hivyo, kuliko utaratibu huu wa serikali wa kuyafungia yote bila kujali
gari lililohusika kwenye ajali," alisema
Mrutu.
Aidha alisema
wanapinga vikali agizo la Sumatra la kuyafungia mabasi 60 ya kampuni 12 kwa
makosa ya kusababisha ajali na wanataka mabasi yanayohusika pekee ndio
yafungiwe.
Alizitaja
kampuni zilizofungiwa mabasi yake kuwa ni Mohamed Trans, City Boy, Ota High
Class, Kisbo Safari, Kisbo Express, Lubonelo na Kanda Safari.
Mrutu pia
alisema kikao kicho kilipinga azimio la serikali kutaka mabasi yanayoenda
masafa marefu kama mikoa ya Mwanza na Mbeya kutumia siku mbili na badala yake
yatumie siku moja kama ilivyokuwa awali.
Alitaja azimio
la tatu kuwa ni kufunga mfumo maalum wa udhibiti wa magari (Car Track System)
ambao utaunganishwa na ule wa Sumatra ili kuliona gari lilipo kwa lengo la
kudhibiti ajali.
Aidha, Mrutu
alisema wamekubaliana mabasi yote yatatembea kilometa 80 kwa saa moja na 50
pale inapohitajika kama kwenye matuta ili kuepuka ajali.
Alisema
wamekubaliana pia dereva atakayehusika kutembea zaidi ya mwendo waliokubaliana,
afukuzwe kazi na kumchukulia hatua stahiki.
"Kama
magari yetu tutayafanyia ukaguzi na pia kufunga kifaa cha kulionyesha basi na
kupunguza mwendo, hakuna haja tena ya kutaka tusafiri zaidi ya siku moja...
maeneo wanayoona kuna hatari ya usalama ni bora yakasubiriana na askari
wakayasindikiza mpaka yanapokwenda,"
alisema.
Aliendelea
kueleza kuwa wamekubaliana Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani,
Mohamed Mpinga, awahakikishie hakuna askari atakayedai mabasi hayo rushwa.
Mrutu alisema
wamekubaliana mabasi yasikaguliwe kila kituo ili kuepuka kupoteza muda wakati
wakisafiri kwenda mikoani ambako kunasababisha madereva kutembea mwendo kasi
ili kuokoa muda waliopoteza njiani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ MABASI YA MIKOANI KUGOMA JUMAPILI.”
Post a Comment