Wednesday, August 17, 2016
NSSF YAIBURUZWA MAHAKAMANI
Do you like this story?
SHIRIKA la
Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limeburuzwa mahakamani na wakazi 87
waliokopeshwa nyumba za mradi wa shirika zilizoko Kijichi jijini Dar es Salaam,
wakiiomba lisiwabugudhi hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.
Kesi hiyo
imefunguliwa na wakazi hao katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi,
wakilalamikia Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF na Kampuni ya Majembe Auction Mart.
Kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana mbele ya Jaji Penterine Kente.
Wakili wa
walalamikaji hao, Benito Mandele, amewasilisha maombi mahakamani hapo kutaka
itoa amri ya kutokubugudhiwa na mazingira ya makazi hayo yabaki kama yalivyo
hadi kesi yao ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Katika kesi ya
msingi, mbali na NSSF, mlalamikiwa wa pili ni Majembe ambaye hakufika
mahakamani. Wakili Mandele alidai kuwa alipeleka wito wa mahakama katika ofisi
yake iliyoko Mwenge, lakini hakufanikiwa kumpata kwa kuwa amehamisha ofisi eneo
hilo.
Jaji Kente
alisema mahakama inatoa hati nyingine kwa ajili ya mlalamikiwa wa pili ili
afike mahakamani kusikiliza kesi dhidi yake. Kesi ya msingi itasikilizwa Oktoba
17, mwaka huu, na maombi ya kutokubughudhiwa yatasikilizwa Agosti 24, mwaka
huu.
Wakazi hao
kupitia kwa wakili wao, waliamua kukimbilia mahakamani kufungua shauri hilo,
baada ya kushindwa kupata ufumbuzi wa madai yao katika Taasisi ya Usuluhishi
kutokana na walalamikiwa kutofika.
Ilidaiwa kuwa
wakazi hao waliamua kwenda katika taasisi ya usuluhishi kutokana na mkataba wao
kuwataka kufanya hivyo kabla ya kuamua kwenda mahakamani.
Kwa mujibu wa
hati ya madai, wakazi hao wanadai kwamba mlalamikiwa wa kwanza (Bodi ya
Wakurugenzi ya NSSF), ameshindwa kutekeleza makubaliano kwa mradi huo kukosa
huduma za kijamii.
Aidha, wanadai
nyumba hizo hazina ubora hali iliyowalazimu wengi wao kutumia fedha zao kufanya
ukarabati.
Wanadai kuwa
kutokana na hali hiyo, baadhi ya wakazi wameshindwa kulipa fedha ambazo
wanatakiwa kulipa kila mwezi, hivyo Majembe walifika na kuwapatia notisi na kuwatangazia
kuwaondoa.
Wakazi hao
wanaiomba mahakama hiyo, kuiamuru bodi hiyo kurejea mikataba, kutambua majukumu
ya msingi ya kila upande na nyumba ziwe za kuwawezesha kuishi na kuwe na huduma
za kijamii.
Katika maombi,
wakazi hao wanaiomba mahakama hiyo kutoa amri ya hali ilivyo kwa wakazi hao
katika makazi hayo ibaki kama ilivyo mpaka kesi ya msingi itakaposikilizwa na
kutolewa uamuzi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ NSSF YAIBURUZWA MAHAKAMANI”
Post a Comment