Saturday, August 13, 2016
RAIS MAGUFULI AISIFIA "SIZONJE" YA MRISHO MPOT, ATEGUA FUMBO LA MASHAIRI YAKE
Do you like this story?
Utunzi
mahiri wa mashairi na ughani uliotukuka wa Mrisho Mpoto, umeligusa sikio la
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye
ameeleza kuwa shabiki mkubwa wa kazi za msanii huyo hususan wimbo wake
‘Sizonje’.
Akizungumza
na Mpoto jana, muda mfupi baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam katika Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Rais Magufuli alimueleza msanii huyo
kuwa anazifahamu vizuri kazi zake na kwamba anaupenda sana wimbo wake wa
‘Sizonje’ huku akichambua baadhi ya mistari iliyomo kwenye beti za wimbo huo.
Mpoto
alikuwa msanii pekee aliyeongozana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa
Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda, Wakuu wote wa Wilaya za Dar es Saalam pamoja na viongozi
wengine waliofika katika uwanja huo wa ndege kumpokea Mkuu huyo wa nchi.
“Nasikiliza
sana nyimbo zako, ila huu wimbo wako wa Sizonje nimeuelewa sana na nausikiliza
kila siku, kwangu umekuwa kama wimbo wa taifa. Mwanzoni nilipata tabu kuuelewa
lakini sasa hivi… aaaah, nimeuelewa vizuri sana. Halafu Sizonje namjua,
nimtaje?,” yalisikika baadhi ya maneno ya Rais
Magufuli kwa Mrisho Mpoto.
Akielezea
tukio hilo lililoleta msisimko wa aina yake uwanjani hapo, Mpoto alisema kuwa
baada ya kumsikia Rais ameanza kuusifia wimbo wake alishtuka na kujawa na
furaha ya aina yake kwani kwa msanii ni jambo la thamani kubwa kusifiwa kazi
yake na Mkuu wa Nchi.
Alisema
kuwa pamoja na kuusifia wimbo huo, Rais alionesha kuufahamu vizuri zaidi baada
ya kuanza kuipitia baadhi ya mistari na kuahidi kumfumbulia fumbo lililofichwa
kwenye wimbo huo watakapokutana tena.
“Unapopata
thamani kutoka kwa Mkuu wa Nchi inaleta faraja sana," amesema Mpoto. "Kwahiyo, mheshimiwa Rais leo
kuniambia kwamba yeye ni shabiki wa kazi zangu na kwamba anapenda sana wimbo wa
Sizonje, na akafunguka kwa mistari ‘minane’ ya Sizonje ikiwa ni pamoja na ile
inayosema ‘huyu mgeni anayepitia madirishani wakati milango ipo!’ Na akaniambia
siku tukikutana ataniambia vile vyumba vitatu kwanini havifunguki,” aliongeza.
Msanii
huyo amemshukuru Rais Magufuli kwa kuthamini mchango wake katika sanaa kwakuwa
anaamini kuthaminiwa ni hitaji kubwa la kila msanii.
“Kwakweli
leo ni siku yenye furaha sana. Najisikia furaha sana. Asante sana mheshimiwa
Rais John Pombe Magufuli. Umenifanya nimekuwa na siku nzuri sana,” Mpoto alifunguka kwa furaha.
Mwaka huu
mwanzoni, Mrisho Mpoto aliachia audio na video ya ‘Sizonje’ aliomshirikisha
Banana Zorro ambapo kwa muda mfupi tu, wimbo huo uligeuka kuwa mkubwa na
kufanya vizuri. Kutokana na ufanisi wa kazi zake, Mpoto ameendelea kukubalika
akipata mikataba ya ubalozi wa mashirika na taasisi kubwa nchini ikiwa ni
pamoja na mfuko wa pensheni wa PSPF.
Mpoto
ambaye mwaka jana alipewa tuzo ya heshima ya WASTA ya nchini Kenya kutokana na
mchango wake katika lugha ya Kiswahili, amejipatia heshima kubwa kutokana na
utunzi mahiri wa nyimbo za awali, zikiwemo Nikipata Nauli, Adela,
Chocheeni Kuni, Samahani Wanangu, Waite, Njoo Uichukue na zingine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RAIS MAGUFULI AISIFIA "SIZONJE" YA MRISHO MPOT, ATEGUA FUMBO LA MASHAIRI YAKE”
Post a Comment