Thursday, September 22, 2016
HALI YA HATARI YATANGAZWA CHARLOTTE MAREKANI KUFUATIA MAANDAMANO
Do you like this story?
Kumezuka maandamano ya watu walio na
hasira katika maeneo ya mji wa Charlotte nchini Marekani, baada ya polisi
kumpiga risasi mwanaume mmoja mweusi, huku kukiwa na maelezo yanayotofautiana
juu ya tukio hilo.
Mkesha wa maombi uliokuwa wa amani,
ghafla uligeuka kuwa maandamo ya watu waliokuwa na hasira, na baadae ukawa
usiku wa vurugu kubwa baada ya mtu huyo kupigwa risasi na kuachwa na majeraha
mabaya sana, huku waandamanaji wakiwavamia polisi waliokuwa wakijaribu
kuwatawanya.
Kumekuwa na maelezo yanayotafautiana
juu ya tukio hilo. Mkuu wa polisi wa mji wa Charlotte, Kerr Putney, awali
aliripoti kuwa mtu mmoja aliyepigwa risasi wakati wa maandamano hayo ameuawa,
lakini maafisa wa mji baadae waliandika katika ukurasa wao wa Twitter kwamba
mtu huyo amepelekwa hospitali na yupo katika hali mbaya
Maafisa hao pia wamesema mtu huyo
alipigwa risasi na raia mwenzake na si polisi. Aidha, afisa mmoja wa polisi
ameripotiwa kuwa anapata matibabu hospitali baada ya kupata majeraha wakati wa
maandamano hayo ya jana usiku.
Mmoja wa waandamanaji Braxton Winston
amerekodiwa akizungumza kwa hasira huku akiwa amezungukwa na waandamanaji
wenzake akimtaka Mkuu wa polisi atoke nje ya jengo aje azungumza nao.
“Daima mnatuambia yale tusioruhusiwa
kufanya. Haturuhusiwi kupiga magoti. Haturuhusiwi kuandamana. Haturuhusiwi
kusimama. Hatuna ruhusa ya kuimba. Kitu gani tunachoruhusiwa kufanya. Chifu
Kerr Putney, toka nje uje utueleze kile tunachoruhusiwa kufanya” amesema
Braxton Winston.
Gavana wa jimbo la North Carolina,
Pat McCrory ametangaza hali ya hatari jana usiku katika mji mkubwa wa jimbo
hilo wa Charlotte, na baadae kuita kikosi cha ulinzi wa taifa baada ya Mkuu wa
polisi wa Charlotte kusema wanahitaji msaada.
Jana usiku, mamia ya waandamanaji
waliokuwa wakipiga mayowe "Maisha ya watu weusi yana thamani" pamoja
na "mikono juu, usifyatuwe risasi" walitawanyika baada ya polisi
kuanza kuwarushia mabomu ya kutoa machozi.
Lakini makundi kadhaa ya waandamanaji
yalibaki, na kushambulia raia, wakiwamo maripota, walivunja vioo vya madirisha
ya mahoteli, majengo ya maofisi, migahawa huku
wakiwasha moto mdogo katika maeneo
tofauti.
Vurugu ziliibuka watu walipoanza
kuuliza masuali mengi kuhusu tukio la Jumanne la kifo cha Keith Lamont Scott,
menye umri wa miaka 43 aliyepigwa risasi karibu na jengo analoishi. Polisi
wamekataa kutoa mkanda wa video wa ushahidi wa tukio hilo lakini wamesema Scott
alikuwa amebeba bunduki na alikataa mara kadhaa kufuata amri za polisi za
kuweka silaha chini. Hata hivyo, familia ya Scott pamoja na majirani zake wanasema
hakuwa amebeba bunduki bali kilikuwa ni kitabu.
Vurugu za Charlotte zimewastaajabisha
wengi, mji huo unaojulikana kwa biashara za mabenki Kusini mwa Marekani, hauna
kawaida ya kutokea vurugu zinazohusiana na ubaguzi wa rangi wa polisi. Mji wa
Charlotte una idadi ya watu wapatao 830,000 na asilimia 35 miongoni mwao ni
watu weusi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “HALI YA HATARI YATANGAZWA CHARLOTTE MAREKANI KUFUATIA MAANDAMANO”
Post a Comment