Monday, September 26, 2016

SIMBA YAINGIA MAFICHONI KUIANGAMIZA YANGA JUMAMOSI




Klabu ya Simba ya Dar es Salaam imeingia rasmi kambini kujiandaa kwa ajili ya mchezo wa ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao wakuu katika soka la Tanzania, Yanga SC.

Mchezo huo wa mzunguko wa saba wa ligi hiyo unatarajiwa kupigwa siku ya Jumamosi Oktoba Mosi mwaka huu, katika dimba la Taifa Dar es Salaam, ambapo Simba imepania kulipa kisasi cha kufungwa na Yanga katika michezo yote miwili ya msimu uliopita wa ligi hiyo.

Meneja wa klabu hiyo Musa Hassan 'Mgosi' amesema maandalizi ya kuchukua point tatu katika mchezo huo yameanza na kwamba tayari timu imeingia kambini ikiwa chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Joseph Omog pamoja na msaidizi wake Jackson Mayanja.

Hata hivyo, Mgosi amekataa kuweka wazi mahali ambapo kambi ya wekundu hao wa Msimbazi imewekwa bila kutaja sababu yoyote.

"Jambo la muhimu ni kwamba watu wajue kuwa timu iko kambini inajiandaa, lakini kujua kambi hiyo iko wapi, siyo muhimu kwa sasa, na tusingependa kuiweka kambi wazi, kama kuna watu wanasema Zanzibar, acha wajue Zanziba, kama Morogoro acha iwe hivyo, lakini sisi tunajua tuko wapi" Amesema mgosi.

Akizungumzia hofu kuelekea katika mchezo huo, Mgosi amesema "tension katika mechi hizi mara nyingi huwa ipo kwa mashabiki na viongozi, lakini kwa wachezaji na benchi la ufundi hakuna hofu yoyote"

Kwa upande wa wapinzani wao, Yanga ambao wamepoteza mchezo wao wa jana mjini Shinyanga dhidi ya Stand United bado hawajaweka wazi kuhusu kambi yao.

0 Responses to “SIMBA YAINGIA MAFICHONI KUIANGAMIZA YANGA JUMAMOSI”

Post a Comment

More to Read