Monday, September 26, 2016

JELA MAISHA KWA KUCHOMA MOTO MAKANISA


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Bukoba mkoani Kagera imewahukumu kifungo cha maisha watu watatu kwa makosa ya kula njama na kuchoma makanisa mbalimbali mkoani hapa.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Emmanuel Manyere alisema licha ya hukumu hiyo, bado watu hao watatu wanakabiliwa na kesi ya kukata makoromeo na mauaji ya watu 16 ambayo inaendelea katika Mahakama Kuu, Kanda ya Bukoba.

Manyere alisema watu hao watatu ambao ni Allyu Dauda, Rashid Mzee na Ngesela Keya walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, mbele ya Hakimu Mkazi wa Bukoba, Victor Biambo.

Alisema washtakiwa hao kwa pamoja wamekutwa na hatia ya kula njama na kuchoma makanisa 16 ya madhehebu mbalimbali mkoani hapa.

Hakimu Bigambo alisema Mahakama imeridhishwa na ushahidi kutoka upande wa walalamikaji na kutoa adhabu ya kifungo cha miaka saba jela kwa wote watatu kwa kosa la kula njama na kifungo cha maisha kwa kosa la kuchoma makanisa.

Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera Augustino Ollomi aliipongeza Mahakama kwa kutenda haki katika kesi hiyo pamoja na kuwataka wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa polisi ili kukomesha vitendo kama hivyo.

Licha ya hukumu katika kesi hiyo namba 67, bado watu hao watatu wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya watu 20 katika maeneo mbalimbali mkoani humo inayoendelea katika Mahakama Kuu, Kanda ya Bukoba.

0 Responses to “ JELA MAISHA KWA KUCHOMA MOTO MAKANISA”

Post a Comment

More to Read