Monday, October 10, 2016

YULE MZEE FUNDI WA KUTENGENEZA RADI SUMBAWANGA AFARIKI, UKITAKA RADI UNAPEWA KWA SHILINGI LAKI 4




MKAZI wa kijiji cha Chipu, Kata ya Kasense, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, Kasiano Ntalasha (80), aliyejijengea umaarufu mkubwa na kuogopeka ndani na nje ya mkoa, ikiwemo nchi jirani ya Zambia kutokana na ufundi wake wa kutengeneza radi, amefariki dunia. 

Mwandishi wa habari hizi alibaini hayo baada ya kufika kijijini humo jana na kuomba kukutana naye kwa mahojiano ndipo wakazi wa kijiji hicho walipoeleza kuwa amefariki dunia miaka miwili iliyopita.

Inasemekana kuwa mganga huyo wa kienyeji kutokana na ujuzi wake huo wa kutengeneza radi alikuwa na wateja kutoka kila pembe ya nchi hii na nchi jirani ya Zambia, walikuwa wakifika kijijini hapo kumuona.

Mkazi wa kijijini humo, Rose Kalazi alidai mteja aliyekuwa akifika kwa mganga huyo ili kupata radi ilimlazimu kutoa fedha taslimu kati ya Sh 400,000 hadi Sh 500,000, iwapo kama angekubaliana na masharti kutoka kwa mganga huyo.

“Mwandishi unadai unataka kupata radi hiyo, je utaweza masharti yake?” Alihoji. “Isitoshe fundi mwenyewe amekufa miaka miwili iliyopita kilikuwa kifo cha kawaida,” alibainisha.

Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho kwa masharti ya kutoandikwa majina yao, wanakiri kuwa tangu kufikwa na umauti kwa mganga huyo visa vya radi kijijini humo havisikiki tena, ambapo hata wale waliorithishwa wanaogopa hasira za wakazi wa kijiji hicho.

“Radi aliyokuwa akitengeneza mganga huyo ilikuwa na uwezo wa kupiga hata msimu wa kiangazi popote pale …..lakini sharti mojawapo alilokuwa akitoa kwa wateja wake ni kwamba lazima anayeenda kuadhibiwa awe kweli ametenda kosa …. Ilitumika pia kutoa onyo kwa mtu aliyeiba au kudhulumu ili aweze kutubu na kurejesha mali aliyoipora au kudhulumu,” alisema mmoja wao.

Simulizi zingine zinaeleza kuwa kijana mmoja alipewa radi na mganga huyo baada ya kudhulumiwa Sh 10,000 aliyomkopesha rafiki yake ambaye baada ya muda wa makubaliano kupita aligoma katakata kumlipa.

“Ndipo alipofika kwa mganga huyo na kupewa radi baada ya kuwa alikuwa ametimiza vigezo kwamba alikuwa kweli amekosewa wakati huo alilipa Sh 2,000, kabla hajapandisha bei hadi kufikia Sh 400,000 au 500,000. Ilikuwa ni radi ya kumuonya “mtuhumiwa’ wake basi radi hiyo iliunguza nguo yake ya ndani na kuwa majivu tena alikuwa akipiga soga na rafiki zake kijiweni mchana kweupe ….alishauri kama kuna yeyote aliyemkosea akamwombe msamaha na amlipe kama anadaiwa,” alisema mmoja wao .

Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, wote walioridhishwa na ujuzi huo wa mganga huyo hawawezi tena kuendeleza kutengeneza radi kwani wakazi wa kijijini humo wamewaonya wakijaribu watabomoa nyumba zao.

0 Responses to “YULE MZEE FUNDI WA KUTENGENEZA RADI SUMBAWANGA AFARIKI, UKITAKA RADI UNAPEWA KWA SHILINGI LAKI 4”

Post a Comment

More to Read